Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (a.s) -ABNA- Katika dunia ya leo iliyojaa misukosuko, ambapo wasiwasi ni mgeni asiyealikwa katika nyoyo za watu, mwenendo wa Mtume wa rehema (s.a.w.w) unatupatia ramani ya hazina ya utulivu. Yeye kwa dua na dhikri aliunda kimbilio salama dhidi ya dhoruba za kisaikolojia.
Kufanya Dhikri / Kumdhukuru Mwenyezi Mungu; Ni Kitulizo cha Nyoyo ambacho Qur’ani imekithibitisha
Mtume Mtukufu (s.a.w.w) katika nyakati ngumu zaidi za msongo, alifanya dhikri / alimdhukuru Mwenyezi Mungu na kufanya Yeye tu kuwa ndiye tegemeo lake. Qur’ani Tukufu inathibitisha kwa uzuri msingi huu:
«الَّذِینَ آمَنُوا وَتَطْمَئِنُّ قُلُوبُهُم بِذِکْرِ اللَّهِ ۗ أَلَا بِذِکْرِ اللَّهِ تَطْمَئِنُّ الْقُلُوبُ»[1]
Yaani: Wale walioamini na nyoyo zao hutulia kwa kumdhukuru Mwenyezi Mungu. Fahamuni kuwa kwa kumdhukuru Mwenyezi Mungu ndiko nyoyo hutulia.
Msisitizo wa Mtume (s.a.w.w) juu ya dhikri kama:
«لَا حَوْلَ وَلَا قُوَّهَ إِلَّا بِاللَّهِ»[2]
(Hakuna uwezo wala nguvu ila kwa Mwenyezi Mungu), hutibu wasiwasi unaotokana na kujihisi dhaifu, na huweka badala yake uwezo usio na mipaka wa Mwenyezi Mungu.
Dua; mazungumzo ya kuponya na Mwenye huruma kuliko wote
Katika mwenendo wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.), dua haikuwa ibada tu, bali ilikuwa nyenzo muhimu ya kusimamia changamoto za kila siku. Alisema:
«الدُّعَاءُ سِلَاحُ الْمُؤْمِنِ»[3]
Dua ni silaha ya Muumini.
Miongoni mwa dua zake za kuondoa mzigo mzito wa wasiwasi alikuwa akisoma:
«اللَّهُمَّ إِنِّی أَعُوذُ بِکَ مِنَ الْهَمِّ وَالْحَزَنِ…»[4]
Yaani: Ewe Mwenyezi Mungu, najilinda kwako dhidi ya huzuni na masikitiko.
Majaalia haya ya karibu huukabidhi mzigo wa kisaikolojia katika mikono ya Mwenye rehema ambaye ana uwezo wa kutatua kila tatizo.
Hujjatul-Islam wal-Muslimin Muhammad Hussein Amin
Mwandishi na mtafiti wa masuala ya dini
-
[1] Surat Ra‘d, Aya 28
[2] Al-Kafi, Juzuu 2, Uk. 553
[3] Bihar al-Anwar, Juzuu 93, Uk. 295
[4] Sahih Bukhari, Juzuu 7, Kitabu cha Dua, Hadithi ya 3.
Your Comment